IMG 4453

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO IMEJIPANGA KUSAIDIA KUTOA MIKOPO KWA WAKULIMA WADOGOWADOGO LAKI TANO (500,000)

1.1 UTANGULIZI

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema imejipanga kusaidia kutoa mikopo kwa Wakulima wadogowadogo walau laki tano (500,000) watoke kwenye kilimo cha kujikimu kupitia miradi ya Kilimo cha umwagiliaji hasa katika maeneo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo.

TADB imeanzishwa kwa madhumuni makubwa mawili ambayo ni:

 1. Kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania;
 2. Kusaidia katika kuleta Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

1.2 Viwango vya Riba vya Mikopo

Katika kutekeleza majukumu yake benki imekuwa ikitoa mikopo ya muda mfupi; muda wa kati; na muda mrefu kwa Wakulima wadogo wadogo, wa kati na wakubwa, hususan kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwenye minyororo ya thamani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugaji nyuki).

Benki imekuwa ikitoa mikopo kwa riba nafuu kama ifuatavyo:

Makundi ya Mikopo Muda wa Mkopo Riba kwa Mwaka
Mikopo kwa Wakulima Wadogowadogo (Smallholder Farmers) Mfupi; Wa Kati na Mrefu 8% – 12%
Mikopo kwa Mashamba/Miradi  Makubwa (Nucleus Farmers, Medium and Large Scale Farmers) Mfupi; Wa Kati na Mrefu 12% – 16%
Mikopo kwa Wanunuzi wa Mazao ya Wakulima Wadogo (Off-takers of Farmers) Mfupi; Wa Kati na Mrefu 15% – 18%
Mikopo ya Ushirika (Syndicated Loans) Mfupi; Wa Kati na Mrefu Kulingana na Riba ya kwenye Soko na Masharti ya Mkopo husika Mkopo wenyewe

 

2.0 MAFANIKIO YALIYOPATIKANA TANGU MEI, 2016 HADI DISEMBA, 2016

 • Benki imekopesha kutoka 1.0 Bilioni hadi 6.5 Bilioni
 • Benki imeweza kukopesha kutoka vikundi vinane (8) hadi vikundi 20
 • Benki imekopesha wakulima 2575 kutoka 944
 • Benki imeweza kuvijengea uwezo vikundi 336 vya wakulima wadogowadogo vyenye jumla wa wanachama 44,400 katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga. Hivyo kuwezesha jumla ya vikundi 19 kutimiza masharti na maandalizi ya msingi ya kuweza kukopa; Vikundi vingine vilivyobaki vinaendelea kupatiwa mafunzo ili viweze kufikia hali ya kuweza kukopesheka.
 • Mafunzo na semina kwa wadau mbalimbali wa kilimo yanaendelea kutolewa na Benki kwa wakulima, viongozi wa vikundi na taasisi pamoja na washirika mbalimbali.
 • Serikali ikishirikiana na TADB imefanya mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kupelekea Bodi ya Benki ya Maendeleo Afrika kutoa kibali cha kuipatia TADB fedha za kukopesha kwenye sekta ya kilimo. Mkataba wa Mkopo umesainiwa Disemba 2016 kati ya AfDB na Wizara ya Fedha na Mipango, ambapo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) inatarajiwa kupatiwa fedha zaidi ya Bilioni 200 kwa ajili ya kukopesha wakulima.

3.0 MALENGO YA KIMKAKATI YA BENKI KATIKA KUSAIDIA KUTOA MIKOPO KWA WAKULIMA WADOGOWADOGO:

 • Benki imepitia upya mpango mkakati wake katika kutoa mikopo ili kuwezesha kufikia wakopaji wengi zaidi ili kuweza kufikia lengo la kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo. Mambo muhimu ya kimkakati yaliyopitiwa upya ni pamoja na; Kuongeza eneo la kijiografia; Bidhaa na huduma zitolewazo; utaratibu wa utoaji mikopo na minyororo ya thamani ya kipaumbele.
 • Kuboresha huduma kwa kuanzisha mazao maalum ya huduma za kibenki kwa wakulima wadogowadogo kulingana na mnyororo husika wa thamani na pia kuboresha huduma za kupitia taasisi za fedha zilizopo ili kufikia Wakulima wengi zaidi.
 • Benki imepanga kupanua wigo wa eneo la huduma na kufika nchi nzima ambapo ofisi sita za kanda na mikoa zitafunguliwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja.
 • Kutoa mikopo ya kuendeleza miradi ya Kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yaliyoainishwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kutanuka nchi nzima kwa utaratibu mahsusi.
 • Kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TADB, mabenki mengine na wadau mbali mbali wa Kilimo hususan wale watakaoshiriki katika hatua mbalimbali za mchakato wa kutoa mikopo. Lengo ni kuchagiza jukumu la TADB la kuwa benki kiongozi ya maendeleo ya kilimo, pamoja na kuhamasisha mabenki na taasisi nyingine za kifedha kutoa fedha kwenye mnyororo mzima wa kilimo.
 • Kuitangaza Benki na Huduma zake kwa Wananchi ili wengi waweze kuzielewa shughuli zake na jinsi benki itakavyowahudumia.
 • Kusimamia utoaji na usimamizi wa fedha kwenye uendeshaji wa miradi ya Kilimo mbalimbali nchini.
 • Kuratibu upatikanaji wa dhamana mbalimbali kwa ajili ya mikopo kwawakulima ili mabenki yaweze kuelekeza nguvu zao kuwakopoesha Wakulima wengi zaidi.
 • Kufanya upembuzi wa miradi ya Maendeleo ya Kilimo na Umwagiliaji nchi nzima ili kubaini mahitaji halisi ya fedha na pia kusaidia kupanga maeneo ya vipaumbele.
 • Kufadhili miradi ya umwagiliaji isiyopungua 20 na teknolojia mbadala 3 kwa maeneo yatakayoainishwa
 • Kukopesha mashamba makubwa (nucleus farms) yasiyopungua 10 yatakayosaidia kuinua wakulima wadogo kutoka kilimo cha kujikumu kwenda cha kibiashara;
 • Kutoa mikopo kwa Wakulima wadogowadogo walau laki tano (500,000) watoke kwenye kilimo cha kujilikmu.
 • Kusaidia uanzishaji wa biashara za kilimo za vijana zisizopungua 1,000 na kuendesha programu za mafunzo 50 kwa vijana.
 • Kufadhili ujenzi wa maghala ya kimkakati katika kila kanda kubwa ya uzalishaji wa mazao ya nafaka
 • Kuendesha mafunzo kwa taasisi za fedha zisizopungua 20, ‘’on-lending institutions’’ 300, na vikundi vya wakulima wadogo wadogo 1,000
 • Kufungua matawi ya Benki katika kila kanda yaani Kanda Sita (6) ikiwemo Zanzibar hadi 2020.

4.0 CHANGAMOTO ZA SHUGHULI ZA UTOAJI MIKOPO

Utoaji wa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi, baadhi ya changamoto hizo ni kama ifuatavyo:

 • Kutokuwa na mvua za uhakika ukizingatia kuwa Wakulima wengi wadogowadogo wamekuwa wakilima kilimo cha kutegemea mvua.
 • Uelewa mdogo wa taratibu za kibenki kwa viongozi wa vyama vya Wakulima wadogowago pamoja na wanachama wanufaikaji wa mikopo.
 • Uelewa mdogo juu ya kanuni za kilimo bora ikiwa ni pamoja na upungufu wa huduma za ugani zitolewazo kwa Wakulima wadogowadogo.
 • Gharama kubwa zinazohusiana na utoaji wa mikopo ya moja kwa moja kwa Wakulima wadogowadogo kulinganisha na mapato ya riba yapatikanayo kwenye mikopo hiyo.
 • Kukosekana kwa masoko ya uhakika kwa Wakulima wadogowadogo, ambapo wanunuzi wengi wakubwa wamekuwa wakisita kusaini mikataba ya ununuzi wa mazao ili kutoa soko la uhakika.
 • Kuchelewa kwa tathmini ya mikopo kunakotokana na upungufu wa taarifa muhimu kutoka kwa vyama vya Wakulima. Pia baadhi ya nyaraka zinazowasilishwa kutokuwa na uwiano sawa kati ya taarifa moja na nyingine.
 • Wakulima wadogowadogo kutokuwa na dhamana za kutosha ili kuweza kudhamini mikopo yao. Pia dhamama zilizopo kutokuwa na usajili wa kisheria kuweza kudhamini mikopo hiyo.
 • Kutokuwepo kwa maghala ya kuhifadhia mazao baada ya mavuno katika maeneo mengi. Hivyo benki inashindwa kuwa na usimamizi mzuri wa mavuno.
 • Wakulima wengi wadogowadogo kutokuwa na kumbukumbu muhimu za uzalishaji wa mazao kwa misimu iliyopita ili benki iweze kufanya tathmini stahiki ya mahitaji ya mkopo kwa waombaji.
 • Kukosekana kwa uadilifu kwa baadhi ya wanufaika wa mikopo na Viongozi kutekeleza wajibu wao ikiwa ni pamoja na marejesho ya mikopo na kupeleka mazao ghalani wakati wa kuvuna.
 • Kuwepo kwa madalali (watu wa kati) katika biashara ya mazao ambao huwarubuni baadi ya wakulima walio kwenye mpango wa mikopo wa Benki.

 

5.0   HITIMISHO

Wananchi hususan wakulima wanaombwa kuwasiliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa anuani na njia nyingine zilizoainishwa hapa chini ili kuweza kupatiwa maelezo ya kina kuhusu huduma zinazotolewa na jinsi ya kunufaika na fursa zilizopo. Pia, TADB inayakaribisha mabenki mengine na wadau mbali mbali wa Kilimo kuchangamkia fursa zinazotolewa na TADB.

 

 

Imetolewa na:

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji,

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *