Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wa Benki Ya Maendeleo Ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (Kulia) Akichangia Mada Wakati Wa Kongamano La Tatu (3) La Sera Kuhusu Kilimo Katika Hoteli Ya Serena, Dar Es Salaam. Kushoto Ni Katibu Mtendaji Wa Mfuko Kichocheo Wa Kuendeleza Kilimo Kusini Mwa Tanzania (SAGCOT – CTF), Dkt. John Kyaruzi.

TADB KUANZISHA MTANDAO WA WADAU KATIKA KILIMO

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imedhamiria kuanzisha mtandao mpana wa majadiliano na wadau mbalimbali, zikiwemo Wizara zinazohusika na Kilimo na Taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi, ili kukubaliana vipaumbele na namna ya kushirikiana katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya TADB.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga wakati akichangia mada wakati wa Kongamano la Tatu (3) la Sera kuhusu Kilimo linaloendelea katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Bw. Assenga alisema kuwa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo kutachagiza kusaidia uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Kilimo, na kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.

Alitolea mfano wa juu ya umuhimu wa ushirikiano na wadau mbali mbali kwa kutaja utekelezaji wa vitendo wa Mkataba wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Morocco kwa kuingi Mkataba na Benki ya Kilimo ya Morocco (yaani Kundi la Utoaji wa Mikopo kwenye Kilimo nchini Morocco) ambayo yamelenga katika maeneo mbali mbali yahusuyo maendeleo ya kilimo, hususan upatikanaji wa fedha.

Aliongea kuwa Benki pia imejipanga kuanzisha majadiliano ya kufunga mkataba wa mashirikiano na tasisi mbali mbali za nje kama ‘Centre for Coordination of Agriculture Research and Development for Eastern and Southern Africa (CCARDESA)’ kwenye miradi inayotekelezwa Tanzania hususan maeneo matatu (Miradi ya Vijana kwenye Bidhaa za Misitu; Miradi ya Vijana na Wanawake kwenye Bidhaa za Mihogo; na Miradi ya Vijana kwenye Masoko kwa kutumia TEHAMA);

Kwa upande wa mikopo, Bw. Assenga, TADB imekuwa ikitoa mikopo ya muda mfupi; muda wa kati; na muda mrefu kwa Wakulima wadogo wadogo, wa kati na wakubwa, hususan kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwenye minyororo ya thamani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugaji nyuki).

Bw. Assenga amesema kuwa mpaka sasa Benki imekopesha jumla ya shilingi 6.5 Bilioni kwa  kukopesha vikundi 20 vyenye jumla ya wakulima 2575.

“Vile vile Benki imeweza kuvijengea uwezo vikundi 336 vya wakulima wadogowadogo vyenye jumla wa wanachama 44,400 katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga. Hivyo kuwezesha jumla ya vikundi 19 kutimiza masharti na maandalizi ya msingi ya kuweza kukopa; Vikundi vingine vilivyobaki vinaendelea kupatiwa mafunzo ili viweze kufikia hali ya kuweza kukopesheka,” aliongeza Bw. Assenga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *